WEKEZA LAKI MOJA UPATE ZAIDI YA MILLIONI MOJA NDANI YA SIKU 90

Na Boniface L. Pwele, Songea.


Leo nataka tuangalie kilimo cha matikiti kibiashara kwa mtaji wa shilingi laki moja tu(100,000/=). Nimeona niandae hili somo kwa kuwa watu wengi hulalamika kuhusu mtaji lakini kwa asilimia kubwa watu humililiki zaidi ya hii pesa laki moja, lakini bado utamkuta analalamika kuhusu mtaji wa kuanzia.


Leo tutaangalia mchanganuo wa shilingi laki moja ili ikuletee milioni moja na nusu(1,500,000/=) kwa makadilio ya chini kabisa hayo ni baada ya siku 75-90 na unaweza pata zaidi ya hapo, ikiwa utaweka juhudi nyingi katika kilimo ambacho unaenda kufanya.


Hapa tutaangalia mchanganuo kwa kutumia mbegu bora ya matikiti aina ya PATO F1. Na eneo linalohitajika ni chini ya robo ekari (yaani nusu ya robo ekari ) ila katika laki moja sijaweka gharama ya shamba ambayo ni nusu ya robo ekari yaani mita 500 za mraba.


Maandalizi ya shamba.


Andaa shamba lenye ukubwa wa mita 500 za mraba( 50m×10m).


Baada ya kuliandaa shamba lako hakikisha una mbolea ya kuku ya kutosha mashimo 500 tu na uhakikishe hiyo mbolea imeoza vya kutosha.


Chimba hayo mashimo 500, chukua mbolea ya kuku ichanganye vizuri na udongo. Kisha  piga dawa aina ya Colt kwenye mashimo ikae walau siku 14.


Baada ya siku ya 14 unaweza panda mbegu zako.


Mbegu ya PATO F1 50g ambayo unaweza kuipata kwa sh 35,000/= tu inatosha kupanda hilo eneo la mita 500 za mraba.


Panda kwa nafasi nzuri, mstari hadi mstari iwe mita mbili na shimo hadi shimo iwe sentimita 50( yaani mita 2 kwa sm 50)


Panda mbegu mbili mbili lakini hakikisha huziweki sehemu moja humo shimoni.


Baada ya kuota mmea ukisha fikisha majani matatu punguza mche mmoja kwa kuukata na siyo kuung’oa.


Matunzo shambani.


Siku ya 0-15 (Planting and germinating) mbegu itakuwa tayari  isha ota na inakaribia kutambaa.


Mmea wa matikiti hupendwa sana na wadudu, hivyo mara baada ya kuota ukiwa na majani angalau matatu tumia dawa ya wadudu aina Prosper 720EC (Profenofos 600g/L + Cypermethrin 120,000/=), ikichanganywa na Agrigrow starter NPK 14:28:18, hii inafanya mmea kuwa na mizizi imara na kuufanya mmea kuweza kufyonza virutubisho vizuri kutoka kwenye udongo,ikichanganywa na Agrilax .


Na hapo uwe na mbolea ya Yara Mila Winner kilo tano ambayo utaweka gramu tano (kisoda kimoja) kwa kila mche


Siku ya 16-25( Vegetative/Trailing)  hapo tikiti litaanza kutambaa hakikisha una Agrigrow vegetative NPK 30:10:10, hii itakuza mmea kwa haraka na kuongeza matawi, dawa ya waduduAvirmec.


Siku ya 25-40 (Flowering) hapo mmea utaanza kutoa maua,hakikisha una mbolea ya Yara Mila Nitrabor ambayo utaweka gram 10 kwa mmea mmoja, dawa ya wadudu Colt, Agrigrow flowering and Fruiting NPK 15:5:35 hii itazalisha maua kwa wingi na kufanya yasipukutike.


Kuwa makini kwenye upigaji wa dawa wakati wa kipindi hiki, inakubidi upulizie dawa asubuhi sana au jioni sana,kwa maana hii hatua ndipo kunakuwa na wadudu wa muhimu shambani kama nyuki,ambaye ni muhimu sana kwa zao hili la matikiti,ndiyo maana unashauriwa kama unalima zaidi hata kama ni ekari moja unaweza weka mzinga wa nyuki shambani kwako ili wasaidie katika uchavushaji.


Siku 41-60-90 (Fruiting) hapo hapo mmea utakuwa umeanza kubeba matunda.


Hatua hii mmea unatakiwa upate maji ya kutosha lakini inatakiwa upunguze kiasi cha maji siku kumi kabla ya kuvuna kulifanya tikiti liweze kutengeneza sukari ya kutosha.


Mavuno.


Kwa eneo la mita 500 mita za mraba (Yaani mita 50 kwa mita 10) utakuwa na miche 1000 kwenye eneo la mita za mraba 500. Kwa kuwa kila shimo itakuwa ni miche miwili. Kumbuka nilikuambia zikiota inabidi upunguze mche mmoja mmoja.


Hivyo katika eneo lako utakuwa na miche 500. Na kwa matunzo mazuri mche mmoja huweza kufikisha hadi matunda matatu. Ila mimi nakupigia kwa hesabu ya tunda moja kwa mche.


Na hilo tunda litakuwa ni kubwa sana kuanzia kilo kumi hadi 15. Kwa matunda 500 na tunda moja kwa kuwa ni kubwa unaliuza kwa bei ya jumla sh 3000/=Matunda 500×3000= 1,500,000/=(Milioni moja na nusu)


Kama utayauza mwenyewe reja reja utayauza kwa sh 5000 hadi 7000 hadi 10,000 kwa tunda moja. Hivyo ukiyauza kwa sh 5000 utaweza kupata 5000×500=2,500,000/=Kumbuka hiyo ni shilingi laki moja imezalisha pesa hiyo ndani ya miezi mitatu (siku 90).


Sasa amua kuendelea kutunza pesa benki ambako makato yanaendelea au uwekeze baada ya miezi mitatu uweze kupata hizo fedha.


Nimeandaa hili somo kukupa mwanga wewe ambaye unatamani kulima lakini unasema huna mtaji na wakati una pesa zaidi ya hii niliyo itaja hapo juu.


Lakini ikumbukwe hyo laki moja sijaweka gharama sijui ya Kukodi hako kakipande ka shamba,kulima unaweza lima mwenyewe kabisa.


Na usiseme sina pesa ya kununua mafuta kwa ajiri ya kumwagilia miche mia tano unaweza chota maji kabisa kwenye ndoo na ukaimwagilia miche yote.


Gharama ya vitu vyote nilivo vitaja hapo juu


Mbegu PATO F1 50g 35,000/=


Agrigrow starter NPK 14:28:18 500g 5000/=


Agrigrow Vegetative NPK 30:10:10 500g 5000/=


Agrigrow flowering and fruiting NPK 15:5:35 500g 5000/=


Yara mila Winner 5kg 10,000/=


Yara Mila Nitrabor 5kg 10000/=


©Dawa za wadudu


Prosper 250mls 9,000/=


Colt 250mls 8000/=


Avirmec 50mls 4000/=


Agrilax 500g 9000/=


Mbolea ya kuku (Omba kwa mtu anayefuga kuku)


Bei za mbolea hizo za Yara inategemeana na wapi ulipo maana unaweza pata chini ya hyo bei.



SHARE THIS
Previous Post
Next Post